Wavamizi Waonywa Juu ya Kujenga Maeneo ya Wazi Yaliyotengwa Maalum kwa Michezo ya Watoto
WATOTO katika kitongoji cha Bogini juu katika kijiji cha Mabogini wilaya ya Moshi vijijini, wameomba mamlaka za vijiji na wilaya kutenga na kuheshimu maeneo kwa ajili ya michezo ya watoto.
Aidha watoto hao wameomba serikali kurejesha maeneo ya wazi yaliyotengwa awali na baadaye kubadilishwa matumizi na kujengwa vibanda vya biashara ama bustani zinazomilikiwa na watu binafsi.
Baadhi ya watoto hao James Masanja, Ally Mohamed na Maria Evarist walisema hawana maeneo ya michezo ya wazi isipokuwa uwanja wa shule ya msingi Benjamin Mkapa ambao ni mali ya tasisisi.
"Kila siku tunacheza katika barabara na viwanja vya watu vya makazi kutokana na kukosa eneo la wazi.... ina maana wamiliki wakijenga, tutakosa kabisa na hii pia inaua vipaji vyetu" alisema Masanja.
[Hili ni miongoni mwa maeneo ya wazi lililopo mtaa wa khambaita kata ya soweto katika manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.]
Naye Mohamed alisema wamekua wakipata majeraha ya kung'oa kucha za vidole vya miguu na hata kukatwa na chupa kutokana na kucheza maeneo yasiyo rasmi.
Kwa upande wao wazazi, Abed Msangi na Swalehe Njama walikiri asilimia kubwa ya makazi yao hayana viwanja vya michezo na. kudai ni jukumu la viongozi kutenga maeneo hayo.
"Nyakati fulani unaweza kudhani eneo lililopo wazi ni la umma lakini badaye unabaini kuwa ameuziwa mtu na kufanya ujenzi wa majengo ya kudumu" alisema Msangi.
[Hili ni miongoni mwa maeneo ya wazi lililopo mtaa wa khambaita kata ya soweto katika manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.]
Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa kitongoji cha Bogini, Bakari Zuber alisema hawajawahi kuuza maeneo ya wazi bali wananchi nao wamekua wakijenga hadi mipakani mwa viwanja vyao.
"Kwa mujibu wa taratibu za makazi ni lazima anayejenga aache angalau mita mbili kutoka nyumba moja na nyingine ili kupata uchochoro utakaofaa pia kwa michezo ya watoto" alisema.
Zuber alisema msimamo wa serikali kuanzia ngazi za vitongozi hadi wilaya ni kuheshimu maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo ya watoto.
Akizungumzia suala Hilo, mwanasheria Evarist Ambros anasema ni wajibu wa wazazi kuhakikisha watoto wanapata mahali pa kucheza kwani ni haki yako kwa mujibu wa sheria ya watoto ya mwaka 2009.