Jinsi Asilimia 60 ya Wanawake Mkoani Mbeya Wajenga Nyumba Wenyewe

Jinsi Asilimia 60 ya Wanawake Mkoani Mbeya Wajenga Nyumba Wenyewe

ASILIMIA  60  ya wanawake mkoani Mbeya, wamefanikiwa kujenga nyumba zao wenyewe kutokana na juhudi walinazo katika kufanya kazi kwa bidii.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ambao alisema asilimia 60 ya wanawake mkoani Mbeya wanaendesha maisha yao bila kutegemea msaada wa mwanaume na kwamba wamefanikiwa kumiliki nyumba zao.

Alisema ukiangalia nyumba zilizojengwa na wanawake ambao kwa kiasi kikubwa ni wajasirimali zinavutia kwa sababu zimezingatia ubora na kiwango kinachotakiwa kwa kuzingatia ramani ya mipango miji inayotolewa na Serikali.

Chalamila aliwapongeza wanawake hao kwa kukubali kupunguza mambo yasiyofaa na kuamua kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba ambayo ni hazina isiyoharibika na itarithiwa  na vizazi.

Wanawake wa Mbeya ni miongoni mwa wanawake Tanzania ambao wanajituma sana katika kutafuta riziki, wanajishughuli na mambo mbalimbali ili kujiongezea kipato ukilinganisha na wanaume ambao asilimia kubwa wanapenda kulelewa, ukionyeshwa nyumba inayomilikiwa na mwanamke utashangaa kwa sababu ya uzuri wake, hakika tuige mfano wao alisema Chalamila.

Aliongeza kuwa kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na ukuaji wa miji , wananchi wanapaswa kujenga nyumba za kisasa ambazo zinavutia miji kuliko ilivyo sasa ambapo katikati ya Jiji la Mbeya zimejengwa nyumba za hovyo.

Aliwataka maofisa mipango miji kuendelea kutoa elimu kwa wananachi wanaonunua ardhi kuhakikisha wanafuata ramani zinazotolewa kujenga nyumba za kisasa badala ya kujiamulia kutumia michoro yao.

Baadhi ya wanawake walisema kuwa siri ya kumiliki nyumba nzuri na za kisasa ni kufanya kazi kwa bidii na kubana matumizi ya fedha inayopatikana.

Miongoni mwa  wanawake  akiwemo Salome Anangisye,  Mkazi wa Isyesye jijini Mbeya, alisema baadhi yao wanapenda vitu vya anasa wanasahau kuwa binadamu anatakiwa kula, kuvaa na kuishi mahali pazuri pa kuvutia.

Alisema miongoni mwa faida za kumiliki nyumba  ni kuondokana na msongo wa mawazo kutokana na madeni ya kodi kwenye nyumba za kupanga lakini kupata amani ya moyo na hewa safi.