Moshi Manispaa Watajwa Vinara Ujenzi Holela

Moshi Manispaa Watajwa Vinara Ujenzi Holela

BAADHI ya wakazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wanatajwa kama vinara wa ujenzi holela usiozingatia mipango miji.

Aidha kutokana na ujenzi huo badhi ya idara za serikali likiwamo jeshi la zimamoto na uokoaji hushindwa kutekeleza majukumu yao hususan yanapotokea majanga kama Moto na mafuriko.

Wakizungumza na Blog hii wakazi wa kata ya Bondeni na Mawenzi, Shaban Kala na Sudi Abdallah walisema ujenzi huo umesababisha vichochoro kuzibwa.

"Utaona baadhi ya mitaa wafanyabiashara ndogo ndogo wamejenga maduka na wengine kuweka vibanda vya biashara, hii inaziba njia za kupita wakati wa dharura" alisema Kala.

Wananchi hao walitaka uongozi wa manispaa kuiga mfano wa aliyekua mkurugenzi wa manispaa hiyo miaka ya 2010, Bernadette Kinabo ambaye alivunja maduka na kuviacha vichochoro wazi.

Kwa upande wake mkaguzi jeshi la zimamoto na uokoaji, Jeremiah Mkomagi alithibitisha manispaa hiyo kuwa ujenzi holela na mara kadhaa ofisi yake imeshindwa kutoa msaada wakati majanga.

Hata hivyo Mkomagi alisema ofisi yake imetoa ushauri kwa halmashauri ili kuboreshwa kwa miundombinu hiyo na hivyo kujenga mji bora na wa kisasa.