Serikali Imeanza Kupima Afya ya Udongo Nchini Tanzania
Mradi wa kupima afya ya udongo nchini unafanywa na kampuni ya OCP kwa niaba ya Serikali. Kwa kuanzia utatekelezwa katika mikoa minne ya Morogoro, Rukwa, Mbeya na Iringa.
Serikali imeanza kupima afya ya udongo nchi nzima kwa lengo la kuandaa ramani maalum itakayo onyesha maeneo ambayo mazao ya aina mbalimbali yanaweza kustawi na kiwango cha mbolea kinachohitajika ili kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija.
Mradi wa kupima afya ya udongo nchini unafanywa na kampuni ya OCP kwa niaba ya Serikali. Kwa kuanzia utatekelezwa katika mikoa minne ya Morogoro, Rukwa, Mbeya na Iringa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii juzi, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya OCP, Dk. Mshindo Msolla alisema wameamua kuanzisha mkakati huo ikiwa ni jithada za kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kupata faida kupitia kilimo.
Alisema maeneo mengi nchini, wakulima hawana elimu juu ya aina gani ya udongo ambayo inafaa kulimwa zao gani na matokeo yake hulima mazao yoyote na kuingia hasara.
"Baada ya kubaini tatizo kwenye afya ya udongo, kampuni yetu imekuja na suluhisho la kudumu kupima afya ya udongo ili sasa kila mkulima katika eneo lake atambue aina ya zao atakalolima kwa kuzingatia matumizi ya mbegu bora, mbolea na watalaam,” alisema Dk. Msolla.
Alisema tayari maandalizi ya kuanza zoezi la upimaji afya ya udongo limekamilika na kwamba wataanza kufanya kazi kwenye mikoa hiyo minne na malengo yao ni kufikia mikoa yote Tanzania ili kuwasaidia wakulima kupata faida katika kilimo kuliko ilivyo sasa ambapo wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Uyole kilichopo mkoani Mbeya, alisema wamepewa jukumu la kutekeleza mradi huo wa upimaji afya ya udongo kwenye mikoa minne.
Alisema kwa kuwa wao ni watafiti wa kilimo wanao uzoefu, hivyo watakwenda kumaliza kabisa tatizo la afya ya udongo kwenye maeneo mbalimbali ya mradi.
Alisema licha ya kuanza zoezi la upimaji wa afya ya udongo, TARI wanaendelea kuwafundisha wakulima matumizi bora ya ardhi, teknolojia za kisasa na kuwapatia wataalam wa kilimo ili kufundishwa namna bora ya kuzalisha mazao yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Kalorius Misungwi aliwapongeza wadau hao kwa kuanzisha mradi wa upimaji afya ya udongo kwa madai kuwa kulikuwa na tatizo kubwa ya virutubisho vya udongo hali iliyosababisha wakulima kupata hasara kwenye mazao yao.
Alisema mradi huo utasaidia wakulima kujua aina za mbegu, mbolea zinazopaswa kutumika kulingana na eneo pindi msimu wa kilimo unapowadia.