Vijana Wa Chuo Cha Uhasibu Arusha Wabuni Mfumo Uitwao 'Pata Estate'
Timotheo Mohamed, Frank Samwel, Anold Kileo na Isack Mboya wanasubiri kukamilisha taratibu kadhaa za kiteknolojia ili mfumo wa Pata Estate uingie sokoni kupitia simu janja (smartphone).
Vijana wa chuo cha uhasibu Arusha (AII) wabuni mfumo (system) inayorahisisha biashara ya kuuza na kununua mashamba, nyumba, viwanja na upangishaji wa nyumba za biashara na makazi.
Vijana hao wanne wanaosoma shahada ya sayansi ya komputa (Bachelor of Computer Science) walipata wazo hilo baada ya kuona kuna changamoto eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wagunduzi wenzake, Timotheo Mohamed alisema kama ilivyokawaida kutafuta majawabu ya changamoto zinazoitesa jamii waliona kuna haja ya kujikita huko.
"Mtu anapotaka kuuza kiwanja, shamba, nyumba au kukodisha analazimika kutafuta madalali ambao mara nyingi wamekuwa wakiwatapeli wanunuzi licha ya kuwapotezea muda" alisema Timotheo.
Alieleza namna mfumo huo uliopewa jina la PATA ESTATE unavyofanya kazi, kuwa muuzaji anaweza kuacha taarifa za kile anachokiuza kwa picha, eneo lilipo (location) na bei huku mnunuzi naye akipata fursa ya kuchagua au kuacha ujumbe wa kile anachokitaka.
"Mfumo wetu unatoa fursa ya kubadili lugha yeyeyote ili kutoa nafasi kwa wageni wanaokuja Tanzania kupata vitu hivyo bila kupita kwa madalali ambao wamekuwa matapeli" alifafanua zaidi.
Mbali na hilo mfumo huu utapunguza gharama kwa makampuni yaliyokuwa yakichapisha vipeperushi au kutangaza kwenye vyombo vya habari biashara ya viwanja, nyumba na mashamba na pia itaokoa muda.
Hata hivyo vijana waliogundua mfumo huo Timotheo Mohamed, Frank Samwel, Anold Kileo na Isack Mboya wanasubiri kukamilisha taratibu kadhaa za kiteknolojia ili uingie sokoni kupitia simu janja (smartphone).