Serikali ya Tanzania Yaridhishwa na Uwekezaji Mashamba ya Ngano, Siha

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na mkurugenzi wa maendeleo ya nafaka katika wizara hiyo Bw. Nyasebwa Chimagu baada ya kutembelea na kukagua kilimo cha mazao hayo katika shamba hilo na kujionea ngano na shayiri ilivyostawi.

Serikali ya Tanzania Yaridhishwa na Uwekezaji Mashamba ya Ngano, Siha
Picha kwa hisani

Wizara ya kilimo imeeleza kuridhishwa na uwekezaji wa kilimo cha mazao ya kimkakati ya kitaifa ya shayiri na ngano katika shamba kubwa la Matadi wilayani Siha mkoani kilimanjaro.

Kadhalika serikali imesema iwapo uwekezaji huo utafanywa katika mashamba yote nchini  yaliyokuwa ya serikali na kuingia mkataba na wawekezaji taifa litafikia malengo ya kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka na kujitosheleza kwa ngano ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na mkurugenzi wa maendeleo ya nafaka katika wizara hiyo Bw. Nyasebwa Chimagu baada ya kutembelea na kukagua kilimo cha mazao hayo katika shamba hilo na kujionea ngano na shayiri ilivyostawi.

Bw. Chimagu, ambaye yupo katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwenye mkutano wa wadau wa ngano na serikali juu ya uzalishaji wa zao hilo atafanya ziara kama hiyo katika mikoa ya Arusha, Manyara na mikoa ya nyanda za juu kusini yenye mashamba makubwa yanayolima zao hilo.

Mwekezaji mzawa wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 342, Bw. Henry Mosha ameipongeza serikali kwa kuwawekea mazingira rafiki wawekezaji na wakulima wa mazao hayo kwa kuingia mikataba na bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko.

Alisema katika makubaliano hayo, serikali inawapatia mbegu na pembejeo na kuishauri serikali kuwa na  utaratibu huo baada ya kuingia mkataba na bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko ili uwe wa kudumu.