Serikali ya Tanzania Yaamua Kuongeza Madarasa Katika Shule za Msingi Kusaidia Elimu ya Sekondari
SERIKALI kwa kushirikiana na wananchi wa Halmashauri ya Wilayaya Mbarali mkoani Mbeya, imefanikiwa kujenga shule mpya za Sekondari sita kwa lengo la kuongeza fursa kwa wanafunzi wanaofaulu mitihani ya darasa la saba, kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Sekondari.
Aidha shule hizo zimejengwa ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa lililojitokeza baada ya idadi kubwa ya wanafunzi kutakiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo ya Mbarali, Ruben Mfune na kubainisha kuwa wananchi wamekuwa na muamko mkubwa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mfune alisema shule zilizojengwa kwa nguvu ya serikali na wananchi ni Shule ya sekondari Muwale yenye madarasa matano, Shule ya sekondari Kapunga yenye madarasa matatu, shule ya sekondari Itamboleo yenye madarasa vitatu, shule ya sekondari Ihanga yenye madarasa matano na shule ya sekondari ya Nyamakuyu yenye madarasa vitano.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ujenzi wa shule hizo ni mwendelezo wa ujenzi wa shule za sekondali na vyumba vya madarasa kwa shule zilizopo na kuwa kwa mwaka 2020 serikali kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kujenga shule mbili ambazo ni shule ya sekondari Ipwani ambayo ilikuwa na madarasa vitatu na kuwa kwa mwaka huu wameongeza ujenzi wa madarasa mawili.
Alisema shule nyingine iliyojengwa mwaka jana ni shule ya sekondari Mwakaganga iliyokuwa na Vyumba vitano na kuwa kwa mwaka huu wameongeza vyumba vingine vitano na kuwa mpango uliopo kwa mwaka ujao ni kujenga shule zingine tatu za sekondari.
Alisema jitihada za ujenzi huo unatokana na mwamuko wa wananchi kutambua mchango wa serikali ya Rais Magufuli katika kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule za awali mpaka shule za sekondari kote nchini.
Alisema mafanikio ya ujenzi wa shule hizo unatokana na michango ya hiyari ya wananchi katika kuharakisha sekta ya elimu wilayani humo,pamoja na mipango thabiti ya wilaya katika kuondokana na changamoto ya wanafunzi wanaokosa elimu kwa sababu ambao zipo ndani ya uwezo wa wilaya.
Mfune aliongeza kuwa mbali na jitihada hizo za wananchi na serikali pia wilaya hiyo ilifanikiwa kuendesha harambee ya wadau mbalimbali wa elimu kuchangia ujenzi wa shule hizo mpya sita za sekondari na ujenzi wa vyumba vingine 36 ambavyo vilikuwa vinahitajika kwajili ya wanafunzi waliokosa nafasi baada ya kuchaguliwa.
“Unajua tulifanikiwa kuendesha harambee ya ujenzi na kupata kiasi cha sh milioni 151 zikiwa ni fedha taslimu na vifaa pamoja na ahadi kwajili ya ujenzi wa shule hizo mpya sita,’’ alisema Mfune
Pia mkuu huyo wa wilaya ya Mbarali amewataka watu ambalimbali kuwekeza katika sekta ya elimu wilayani humo kwa kujenga vyuo vya aina mbalimbali kwa kuwa wilaya hiyo inajitosheleza katika masuala ya kiuchumi kutokana na kilimo cha zao la mpunga.
Alisema kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita wilaya hiyo ilikuwa ikisuasua katika suala la elimu kutokana na kuwa wengi wa wananchi walikuwa wanathamini zaidi kilimo na ufugaji badala ya elimu na kuwa kwa sasa kuna mabadiliko makubwa kutokana na juhudi za serikali ya wilaya,mkoa na taifa kuhamasisha sekta ya elimu wilayani humo.