Serikali ya Tanzania Yatoa Miezi Mitatu Kuthibitisha Umiliki Ardhi
TANZANIA imetoa Muda wa miezi mitatu kwa wananchi, Vikundi, Taasisi na kampuni kujitokeza katika ofisi za ardhi za wilaya na mikoa ili kuhakiki umiliki wa ardhi zao.
Katibu mkuu wa wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo ameeleza hayo katika taarifa yake kwa umma kuhusu Muda maalum wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Katika taarifa yake iliyochapishwa katika tovuti ya wizara hiyo, imeeleza kuwa wananchi, taasisi na kampuni mbalimbali nchini zinapaswa kuwasilisha taarifa za ardhi kuanzia Julai mosi hadi September 30 mwaka huu.
Taarifa hiyo imeeleza zoezi la uhakiki wa taarifa za wamiliki wa ardhi litaratibiwa kwenye Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kote nchini.
Makondo ameeleza kuwa Wamiliki wote wa ardhi wanatakiwa kujaza taarifa zao za umiliki wa ardhi kwenye dodoso maalum linalopatikana katika ofisi tajwa au kwenye tovuti ya Wizara (www.lands.go.tz)
Aidha wizara imesema wanaokwenda kuhakiki ardhi zao wanapaswa kuambatanisha Vivuli vya Hatimiliki au Barua ya Toleo au Leseni ya Makazi.
Vingine ni pamoja na Kivuli cha Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au namba ya NIDA na iwapo mmiliki ni Kampuni au Taasisi awasilishe Vivuli vya Hati ya Usajili, taarifa za wanahisa na Vitambulisho vya Taifa vya wanahisa.
Wamiliki wa ardhi ambao watashindwa kuwasilisha taarifa zao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali, wanaruhusiwa kuwasilisha taarifa kupitia kwa wawakilishi wao ambao
Watawatambulisha kwa barua rasmi.