Viongozi wa Vijiji Waonywa Juu ya Ugawaji Holela wa Ardhi
VIONGOZI wa vijiji wameshauriwa kufuata taratibu za kisheria katika kugawa ardhi ya vijiji kwa wawekezaji ikiwemo kuwashirikisha wananchi badala ya kujiamulia wenyewe ili kuepuka kuibua migogoro kati ya wananchi na wawekezaji.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Ofisa Mipango Miji kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Enock Kyando, wakati alipokuwa anatoa elimu ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji vya Uturo, Mtamba, Ukwama na Kapunga wilayani Mbarali.
Kando ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Maalumu ya uelimishaji wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi na ujirani mwema, alisema Mkutano Mkuu wa Kijiji ndio wenye Mamlaka ya kugawa ardhi ya Kijiji.
Alisema kazi ya viongozi wa vijiji hasa Ofisa Mtendaji na Mwenyekiti ni kupokea maombi ya wanaotaka kupewa ardhi na kuitisha mikutano ya vijiji ili wananchi wajadili na kuridhia ama kutoridhia kugawa ardhi yao kulingana na uhitaji.
“Msimamizi Mkuu wa ardhi ya kijiji ni wanakijiji wenyewe na ndio wanaotakiwa kuamua kumpa mtu mwingine ardhi yao kwa ajili ya matumizi ambayo wataona wao inafaa, kiongozi ukifanya maamuzi mwenyewe unasababisha migogoro,” alisema Kyando.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya ardhi, Kijiji kinaruhusiwa kugawa ardhi isiyozidi Hekta 50 kwa mtu mwingine na kwamba ikizidi ukubwa huo zipo mamlaka zingine ambazo zinahusika na hivyo mhitaji wa ardhi hiyo atatakiwa kuziona.
Kuhusu mpango wa matumizi bora ya ardhi, Kando alisema kila kijiji kinatakiwa kuwa na matumizi bora ya ardhi kwa maelezo kuwa utaratibu huo unasaidia kupuondoa migogoro ya ardhi kwa kuepusha mwingiliano wa shughuli za kibinadamu.
Alisema katika kipindi hiki ardhi ni muhimu na inahitaji usimamizi wa karibu na kwamba bila hivyo kuna hatari ya kutokea vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Vilevile aliwashauri wananchi kumiliki ardhi yao kisheria kwa kuyatafutia hati miliki ili kuwa na uhalali wa kuitumia kama dhamana wakati wanapokopa fedha kwenye taasisi za kifedha.
Kwa upande wake Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mbarali, George Mwaijobelo, alisema Wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na migogoro mingi ya ardhi kutokana na vijiji vingi kutokuwa na matumizi bora ya ardhi.
Alisema kutokana na elimu ambayo Kamati yao inaitoa kwa wananchi baadhi ya vijiji vimeanza kuwa na uelewa na kwamba vijiji hivyo vimeanza kupanga matumizi bora ya ardhi.
“Ardhi yetu haiongezeki lakini binadamu tunaongezeka na mifugo yetu inaongezeka, kwahiyo ni lazima tuwe na matumizi bora ya ardhi kulingana na shughuli zetu za kiuchumi na kijamii,” alisema Mwaijobelo.
Alisema baadhi ya maeneo yanatakiwa kutengwa kwa ajili ya kilimo, makazi, kuchungia mifugo na shughuli zingine za kijamii ikiwemo maeneo ya viwanda na taasisi za Serikali.
Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo waliishukuru Serikali kwa kuanzisha utaratibu huo wakidai kuwa utawasaidia kumaliza migogoro ya ardhi ambayo walidai imezidi katika Wilaya hiyo.