DC Mbarali Apiga Marufuku Ranchi ya Usangu Kukodishwa Kwa Ajili ya Kilimo

Imebainishwa kuwa mgogoro ulikuwepo baina ya wawekezaji wa Ranchi ya Usangu na wakulima waliopangishwa.

DC Mbarali Apiga Marufuku Ranchi ya Usangu Kukodishwa  Kwa Ajili ya Kilimo

SERIKALI wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya, imepiga  marufuku wawekezaji wa Ranchi ya Taifa (NARCO) kukodisha mashamba ya Ranchi ya Usangu ) kwa ajili ya  shughuli za  kilimo cha Mpunga.
 
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune ametoa maagizo hayo kwa niaba ya waziri wa Mifugo na Uvivu, Ndaki Mashimba alipofanya ziara katika Ranchi hiyo kujionea shughuli zinavyofanyika. Baadaye alizungumza na wananchi wa kata za Mwatega na Ruiwa  ili kufahamu Ranchi hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Imebainishwa kuwa mgogoro ulikuwepo baina ya wawekezaji wa Ranchi ya Usangu na wakulima waliopangishwa ambapo kwa wakati huo walidai kukodishana mashamba kwa ajili ya kilimo cha Mpunga.

Wawekezaji walikodisha mashamba kwa wakulima kwa gharama kubwa ukilinganisha na ile waliyoitoa wao kwa uongozi wa NARCO.

“Nimeelekezwa na  Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuwa wakulima wote waliopangishwa na kulima ndani ya Ranchi ya Usangu waachiwe mazao yao na wasitozwe tozo yoyote hadi watakapovuna na wasirejee tena kwani sehemu hiyo ni kwa ajili ya ufugaji na kuzalisha malisho ya mifugo. Ni marufuku kwa wawekezaji kufanya biashara ya ukodishaji wa ardhi ya Ranchi kwa kulima na hakuna shughuli zozote za kilimo zinazoruhusiwa kufanyika katika Ranchi za Taifa, hatua zitachukuliwa kwa wawekezaji watakaoendelea kuwakodisha wakulima kwa kuwafutia mkataba.” alisema Mfune.