DC Mbeya Ashauri Mafundi Kukopeshwa Fedha za Halmashauri Kununua Vifaa vya Ujenzi

DC Mbeya Ashauri Mafundi Kukopeshwa Fedha za Halmashauri Kununua Vifaa vya Ujenzi

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Wiliam Ntinika amezishauri Wilaya zote za  Mkoa wa Mbeya kuwa asilimia 10 ya fedha za Halmashauri  zilizotengwa kwa ajili kuviwezesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, ziwanufaishe pia vijana wenye ujuzi wa ujenzi wa vyoo bora.

Ntinika aliyasema hayo jana wakati wa kuhitimisha mradi wa kuwajengea uwezo vijana wa Halmashauri tatu ikiwemo Mbarali, Chunya na Mbeya, namna ya kutumia ujuzi wa kujenga vyoo bora kibiashara.

Alisema Halmashauri zitoa kipaumbele kwa vijana 121 waliopata elimu ya ujenzi wa vyoo bora baada ya kupata ufadhili na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Catholic Relief Services kwa kushirikiana na Human Development Innovation Fund kugharamiwa mafunzo ya Ufundi Veta ili kujenga vyoo vilivyokidhi vigezo.

“Vijana hawa wapewe mikopo ya vifaa vya ujenzi ili wafanye kazi zao  bila vikwazo vyovyote, tuendelee kuwahamasisha waliopata ujuzi huo wajiunge kwenye vikundi ili wanufaike na maofisa maenedeleo wawatambue,”alisema Ntinika.

Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Christopher Mathias alisema kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 jumla ya vyoo 234 vimejingwa kwenye Kata za Maendeleo, Igoma na Tembela.