Waziri Lukuvi Awakumbuka Wananchi Maskini Kupata Hati Miliki

Waziri Lukuvi Awakumbuka Wananchi Maskini Kupata  Hati Miliki

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imefanikiwa kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi wa ardhi kwa kuvunja kanda zote nane za Makamishna wa Ardhi nchini na kuanzisha usimamizi mpya kwa kupeleka Kamishna wa Ardhi katika kila mkoa lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

Moja ya ziara zake akiwa mkoani Mbeya, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema uamuzi huo ni kuendelea kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21).

Alisema hatua hiyo itasaidia kuratibu na kusimamia upangaji ambao unalenga kuwa na miji na makazi bora yaliyopangwa, kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kufuatilia utekelezaji wake na kuwa na uhakika wa uwekezaji katika ardhi.

“Tumeanza utekelezaji wa kuanzisha hizi kanda nane kwa hiyo tutakuwa wawakilishi wa kila mkoa, na tunaanzisha rasmi Ofisi ya Ardhi ya Mkoa na ndani ya ofisi hiyo kutakuwa na mtu anayeratibu mambo ya mipango miji, upimaji wa ardhi, utoaji wa hati miliki za ardhi zikiwemo  za kimila, masuala ya usajili wa hati, nyaraka na miamala ya ardhi na uwekaji wa mifumo ya upatikanaji wa makazi bora na kwa gharama nafuu na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi, ” alisema Lukuvi.

Alisema kuwa kila Halmashauri inayohitaji kufanya mabadiliko ya mipango miji, itaishia katika ngazi ya mkoa na haitatakiwa kwenda katika ngazi ya Kanda kama ilivyokuwa awali.

Lukuvi alisema kuwa lengo la Serikali kuchukua uamuzi huo ni kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa imebaini kuwa suala la umbali limekuwa ni kikwazo kikubwa cha wananchi kupata hati zao za umiliki wa ardhi.

Alisema awali kulikuwa na mrundikano mkubwa wa hati za umiliki wa ardhi kwenye ofisi za makamishna wa Ardhi wa Kanda ambazo hazijachukuliwa na wananchi na baada ya uchukunguzi imebainika kuwa walioshinda kufika kuzichukua wananishi mbali na ofisi hizo.

“Mpaka hivi sasa ninavyozungumza kuna hati miliki za ardhi zaidi ya milioni 20 kwenye ofisi zetu za Makamishna wa Ardhi nchi nzima hazijachukuliwa, tumebaini hii inatokana na umbali maana mwananchi aliyepimiwa ardhi yake kule Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi anapaswa kwenda kuchukua hati yake kwenye ofisi ya Kamishna wa Ardhi wa Kanda mjini Tabora, inawezeka kabisa akawa hana  fedha ya kumfikisha Tabora na ndio sababu tunahitaji sasa huduma hizi azipate kwenye mkoa wake,” alisema Lukuvi.

Akifafanua zaidi alisema kuwa ndani ya Ofisi ya Ardhi ya Mkoa kunakuwa na kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi, hivyo hata hati ya umiliki wa ardhi itatolewa katika ngazi ya Mkoa.

Alisema kwa vile nchi inakoelekea itakuwa na mfumo mpya wa utoaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa njia ya kielektroniki, hata saini ya Kamishna Mkuu wa Ardhi itakuwepo kwenye mfumo, hivyo hati zote zitakazotolewa katika ngazi ya mkoa zitakuwa zimesainiwa na Kamishna Mkuu wa Ardhi.

“Katika Ofisi hizi za Ardhi za Mkoa hakuna kitu kitakachokuwa nje ya uwezo wenu, mtafanya kila kitu na kazi ya Wizara itabaki kuratibu tu mfumo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri,” alisisitiza Lukuvi.

Akizungumzia Mfumo mpya wa ukusanjaji kodi ya Ardhi, Mthamini Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Evaline Mugasha alisema lengo la Serikali ni kuwa na mfumo mmoja wa kukusanya kodi ya ardhi nchi nzima.

Alisema mfumo huo utawashirikisha wadau wote wa ardhi, kuanzia wachora ramani, wapimaji mpaka kwa watoaji wa hati miliki ili kuhakikisha hakuna kipande cha ardhi nchini ambacho hakitakuwa kinalipiwa kodi.

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Thadei Kabonge alisema mfumo huo pia utasaidia kuondoa kabisa migogoro ya ardhi nchini.