Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Yaeleza Mikakati Kuboresha Huduma
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inatarajia kukusanya, Shilingi Bilioni 200 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo, kodi ya pango la ardhi, ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na Sekta ya Ardhi kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Kwa mujibu wa ripoti ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisomwa katika Bunge la Tanzania mwaka 2020, Waziri William Lukuvi alisema lengo la kukusanya fedha hizo ni kuimarisha miundombinu ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri itakayosaidia ukusanyaji wa mapato kwa urahisi.
Kuboresha kanzidata ya wamiliki wa ardhi kwa kutumia mfumo unganishi wa kielektroniki utakaosaidia kuhifadhi kumbukumbu za ardhi na kuwasiliana na wamiliki kwa urahisi kupitia mawasiliano ya simu na barua pepe.
Kushirikiana na Serikali za Mitaa kusambaza hati za madai, kufuatilia malipo ya madeni na kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kwa mujibu wa sheria.
Kuongeza wigo wa makusanyo kwa kuwahamasisha wananchi kumilikishwa viwanja vilivyopimwa pamoja na kutambua 18 na kusajili wamiliki wa kila kipande cha ardhi katika maeneo ambayo hayajapangwa na kupimwa.
Kupima maeneo ya uchimbaji wa madini na kutoza kodi stahiki; vi) Kuhakiki matumizi ya ardhi iliyomilikishwa yakiwemo maeneo ya taasisi za umma na za kidini ili sehemu ya ardhi inayotumiwa kibiashara itozwe kodi stahiki.
Kuweka utaratibu wa kutoza kodi ya pango la ardhi kwa mashamba makubwa yanayotumika kibiashara, kutambua na kutoza kodi wamiliki wenye Hatimiliki za Sehemu ya Jengo (Unit Titles) na kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa wamiliki wa ardhi kulipa kodi kwa wakati.
Aidha ripoti hiyo ilifafanua kuwa dhamira ya Serikali kuifanya ardhi kuwa kichocheo cha maendeleo na nyenzo muhimu katika kupambana na umaskini na kwamba ili kufikia azma hiyo, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na sekta ya ardhi ili wananchi waweze kuitumia ardhi kwa tija.
“Wizara inaendelea kuhamasisha na kufuatilia wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, nawapongeza wamiliki wa ardhi waliolipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati lakini pia natoa rai kwa wananchi waliopimiwa ardhi, kutambuliwa milki zao na kumilikishwa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka tozo ya adhabu au hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao,” alisisitiza Lukuvi.
Akizungumza kuhusu usimamizi wa sekta ya ardhi, Waziri Lukuvi alisema utawala wa ardhi unalenga kuhakikisha ardhi yote nchini inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kwa lengo la kuboresha huduma katika uwekezaji, uboreshaji wa makazi na kuwa kichocheo cha kuinua uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Alisema majukumu hayo yanatekelezwa kwa mujibu wa sera, sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza sekta ya ardhi sambamba na kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa huduma za sekta ya ardhi zinapatikana karibu na wananchi ili kuwapunguzia usumbufu na gharama za upatikanaji wake.
“Pamoja na juhudi hizo, bado wananchi wamekuwa wakipata usumbufu na kutumia gharama kubwa kuzifikia ofisi hizo kwa muktadha huu, Wizara imeanzisha Ofisi za Ardhi katika Mikoa yote 26 nchini ambapo huduma zote za upangaji, upimaji, umilikishaji, uthamini, usajili wa Hati na 22 Nyaraka, ramani na michoro zitapatikana katika ofisi hizo,” alisema Lukuvi.
Aliongeza kuwa Wizara itaendelea kuzipatia ofisi hizo vitendea kazi, rasilimali fedha pamoja na watumishi wa kada zinazohitajika ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Katika mwaka wa fedha 2019/202O Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iliahidi kuhuisha ramani za msingi 68 pamoja na ramani nyingine katika wilaya mbalimbali.
Hadi kufikia 30 Aprili, 2020, ramani za msingi 68 zenye uwiano wa 50,000 na ramani za Mikoa 23 zilihuishwa na kwamba mwaka wa fedha 2020/2021 itaendelea kuhuisha ramani za msingi 66 katika wilaya mbalimbali nchini.