Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Aomba Kupitiwa Upya Mchakato Kugawa Manispaa Jijini Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Aomba Kupitiwa Upya Mchakato Kugawa Manispaa Jijini Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amesema  wanaangalia upya mapendekezo ya kulifanya Bonde ya Uyole kuwa Manispaa kutokana na jiografia na vigezo vingine kufanyiwa kazi haraka.

Mkakati wa kuigawa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa Manispaa mbili,  ulianza mwaka jana baada ya Hayati Dk. John Magufuli wakati wa kampeni zake,   aliwaahidi wananchi wa Mbeya kuwa lazima jiji la Mbeya ligawanywe ili kuboresha na kusogeza huduma kwa wananchi waishio pembezoni.

Chalamila alisema baada ya mchakato kuanza vikao mbalimbali vimekaa kwa ajili ya majadiliano kupitia baraza la Madiwani,Watendaji wa kata, vijiji, viongozi wa vyama vya siasa na machifu kutoa mapendekezo yao ambao wote walibariki Halmashauri ya Jiji la Mbeya ligawanywe na kuwa na Manispaa mbili.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wananchi wa Kata ya Igawilo, Chalamila alisema Manispaa zilizopendekezwa ni Manispaa ya Jiji la Mbeya na Manispaa ya Uyole,  ambazo zote zimegawanywa kwa kutumia Kata kwa mujibu wa ramani iliyochorwa na wataalam wa mipango Miji.

“Hatujafikia maamuzi ya mwisho kuhusu kuzigawa hizi manispaa kwa sababu bado mapendekezo yanaendelea kutolewa kuna vitu vya msingi inatupasa tuviangalie cha kwanza ni jiografia ya bonde la Uyole, miundombinu mengine ambayo itakuwa kiunganishi  rahisi ili wananchi wapate huduma kwa wakati  kuliko ilivyo sasa ambapo kuna mpanglio mbaya wa makazi ya wananchi,” alisema Chalamila.

Aliongeza kuwa tayari viwanja 528 vimepimwa katika Kata ya Iduda na kwamba fidia kwa wananchi itakuwa ni zaidi ya shilingi Bilioni moja na kwamba tayari wameanza kulipa fidia hizo.

Alisema hadi sasa wanadaiwa kiasi cha shilingi Milioni 400 ili kumaliza kulipa fidia  kwa wananchi na kwamba wiki hii watatoa tangazo ili vianze kuuzwa.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Mbeya ,Dormohamed Issa alisema madiwani kwa kushirikiana na Mkurugenzi wataendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujenga na kuanzishwa ili kuchochea uchumi wa Jiji hilo.

Alisema miongoni mwa miradi wanayoendelea kuisimamia kikamilifu ni pamoja na Ujenzi wa Hospitali teule ya Igawilo ambao unaendelea kujengwa na kuboresha majengo mengine ili  huduma za matibabu zitolewe kwenye mazingira mazuri.

 Aliwaomba wananchi wa Mbeya, kutoa ushirikiano pindi wanapobaini viashiria vya rushwa katika miradi inayoendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali ya Jiji ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.