Manispaa ya Moshi Yatishia Kubomoa Majengo yote Yanayojengwa Mwishoni mwa Wiki

Manispaa ya Moshi Yatishia Kubomoa Majengo yote Yanayojengwa Mwishoni mwa Wiki
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi, imesema itabomoa bila kulipa fidia majengo yote katika manispaa hiyo ambayo yanajengwa mwishoni mwa wiki na siku za sikukuu kukwepa mkono wa sheria unaotaka kujenga majengo ya ghorofa.
 
Aidha Manispaa hiyo, inatarajia kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa mitaa na kata ambao wanashuhudia ujenzi wa majengo hayo bila kujiridhisha kama kuna vibali ama la.
 
Meya wa manispaa ya Moshi Juma Raibu alitoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi wakiituhumu manispaa hiyo kuwalinda baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wakubwa ambao kwa makusudi wameendeleza ujenzi huo.
 
Alisema ni msimamo wa Manispaa kusimamia sheria zinazozuia matumizi holela ya ardhi, ujenzi usiozingatia mipango miji na uvamizi wa maeneo ya wazi.
 
"Tayari manispaa imesimamisha ujenzi katika kata  za Mawenzi na Korongoni na kwamba wahusika wamekimbilia mahakamani, sitawezi kulijadili jambo hili kwa kina lakini kimsingi tumezimamisha ujenzi wa nyumba nne ndani ya eneo la manispaa"alisema.
 
"Kuna tabia ya baadhi ya wakazi ambao wanatumia ujanja wa kujenga majengo yao mwishoni mwa wiki na sikukuu ambazo kimsingi ni siku za mapumziko kwa watumishi wa umma...nimeelekeza watendaji hao watoe taarifa na manispaa itachukua hatua"alisema.
 
Kwa upande wake diwani wa viti maalum kata ya Bomambuzi, Faidha Hemed alisema atashirikiana na wenyeviti wa mitaa kuhakikisha wanatoa taarifa katika mamlaka husika kwa wale wanaotumia ujenja wa kujenga nyumba ndani kwa kubomoa kuta moja moja.
 
"Wapo baadhi ya wananchi wanabomoa nyumba zao na kujenga kuta moja moja kama vile wanaziba nyufa lakini katika ukweli halisi wanafanya ukarabati aidha wa kuondoa nyumbaa za udongo na kujenga za kisasa lengo likiwa kukwepa sheria inayowataka kujenga ghorofa"alisema.
 
Katika malalamiko yao, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Moshi, wameelezea kusikitishwa kwao na mfumo wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuendeleza majengo yao katika eneo la manispaa hiyo bila kufuata kanuni\zinazotaka kujengwa kwa majengo ya ghorofa.
 
Aidha wananchi hao walidai kuna uwezekano wa wafanyabiashara hao wakawa wanalindwa na Manispaa ingawa ujenzi huo ukifanywa na wananchi wa kawaida majengo yao hubomolewa mara moja.
 
Katika mahojiano kati ya bwana, Zephania Kessy, Ali Mustapher na Abel Mzava walitaka sheria za manispaa kufuatwa bila upendeleo ama baadhi kulindwa na wengine kuonekana wanavunja sheria.
 
Wametaja kata za Kiusa, Bondeni, Korongoni na Mawenzi ambazo wameshuhudia kuwapo kwa majengo yaliyokuwa ya udongo lakini yamejengwa kinyemela na kujengwa fremu za maduka kinyume na sheria za manispaa zinazotokana maeneo hayo kujengwa nyumba za ghorofa.