Mikakati ya Kupima Ardhi Jiji Mbeya Yaanza

Mikakati ya Kupima Ardhi Jiji Mbeya Yaanza

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imeanza mikakati ya kupima ardhi katika Kata ya Mwansekwa ikiwa ni utekelezaji wa mpango kabambe wa Jiji hilo ambao ulibuniwa hivi karibuni kwa lengo la kukabiliana na ujenzi holela wa makazi.

Mkakati huo umeanza kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida ya upimaji wa ardhi hiyo pamoja na mpango kabambe wa Jiji hilo ambao umeanza kutekelezwa.

Akiwasilisha mpango kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika kata hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya, Amede Ng’wanidako alisema mabadiliko ni lazima yafanyike kwa sababu mji unakua kwa kasi.

Alisema pamoja na kutaka kuupanga vizuri mji lakini pia kitendo cha kupima ardhi ya wananchi kinasaidia kuiongeza thamani kwa maelezo kuwa uwanja uliopimwa bei yake ni tofauti ni kubwa kuliko ambao haujapimwa.

“Halmashauri ya jiji la Mbeya imekuja na mkakati wa kupima ardhi katika maeneo mbalimbali,leo tuko kata ya Mwansekwa  kwa ajili ya zoezi hili na tutapima maeneo yote yaliyo kwenye mkakati kabla ya kufanya hivyo tutatoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa zoezi hilo,” alisema Ngw’anidako.

Aliongeza kuwa wananchi wote lazima washirikishwe kwenye mchakato huo kuanzia hatua za awali hadi kwenye zoezi la upimaji ardhi  ili kutambua malengo ya serikali kutekeleza katika  eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya William Ntinika aliwatoa hofu wananchi wa Mwansekwa  na kuwaahidi kuwa kila mwenye ardhi  atapatiwa haki yake.

Alisema zoezi  hilo la upimaji ardhi litawapa kipaumbele kwa wamiliki wa ardhi wa asili kwa kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki zake huku akiutaka uongozi wa kata kutoa elimu zaidi  juu ya umuhimu wa upimaji ardhi.