Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Yatoa Maagizo kwa Wizara
Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi,Maliasili na Utalii imeitaka Wizara ya Maliasili na Utalii iendelee kuboresha miundombinu ya mawasiliano na huduma za malazi kwa ajili ya watalii wa ndani na nje ya nchi katika hifadhi zote za Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Aloyce Kwezi ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati wa kikao cha majumuisho ya wajumbe wa kamati hiyo baada ya kutembelea hifadhi Taifa ya Nyerere na mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi .
Amesema hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Bwawa la Nyerere ambalo litakuwa ni kivutio kikubwa cha Utalii ujenzi wake upo katika hatua nzuri hivyo Wizara ya Maliasili na ianze kuweka mikakati ya kuweka miundombinu mipya na kuboresha iliyopo.
“ Suala la mawasiliano kwenye hifadhi za taifa ni lazima liboreshwe ili kuhamasisha na kutangaza utalii kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau wa utalii kutokana na kuwepo kwa tatizo la mawasiliano wanapokuwa hifadhini” amesema Mwenyekiti huyo.
Dkt. Kwezi amesema ni vyema Wabunge wakawa mstari wa mbele katika kutembelea hifadhi zilizopo huku wakihamasisha wananchi kufanya utalii wa ndani badala ya kuona utalii ni kwaajili ya wageni wa kutoka nje pekee.
Mwenyekiti huyo na wajumbe wa kamati hiyo wamepongeza jitihada zilizofanywa za uboreshaji wa miundombinu pamoja na makazi kwaajili ya utalii katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
“ Kipekee nipongeze hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa kuwa miongoni mwa hifadhi zenye miundombinu inayofika kiurahisi wakati wa masika na kiangazi” amesema Dkt. Kwezi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema Wizara itahakikisha maagizo yote na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo yanatekelezwa na kufanyia kazi kwa wakati ili kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.
“ Tumepokea maagizo ya Kamati ya Bunge hasa kuzifanyia kazi changamoto za mawasiliano kwenye baadhi ya hifadhi zetu, tutahakikisha mawasiliano yanaboreshwa katika hifadhi zetu hapa nchini” amesema Mhe Mary Masanja.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Dkt. Allan Kijazi,akizungumzia matukio ya ujangili katika hifadhi za Taifa amesema kuwa Wizara imeweza kudhibiti kwa kiwango kikubwa katika hifadhi ikiwemo ya Mikumi .
Dkt Kijazi amesema katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi tangu mwaka 2017 mpaka sasa hakukuwa na matukio ya ujangili wa tembo akieleza kuwa vilivyobaki sasa ni vitendo vya baadhi ya watu kutafuta vitoweo.
Hata hivyo amesema Wizara pamoja na Mashirika yake yanayosimamia maeneo ambayo yamehifadhiwa imejizatiti kutumia Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu kuhakikisha wanatokomeza ujangili kwa asilimia 100 katika maeneo yote.
“Niwaombe wadau na wananchi kwa ujumla tushilikiane ili kutimiza azma ya wizara kutokomeza ujangili katika maeneo yetu yote ambayo yameifadhiwa"amesema Dkt. Kijazi.