Wakazi wa Jiji la Dar es salaam Wachoshwa na Madalali
Wananchi wa jiji la Dar es salaam wamechoshwa na mfumo wa madalali ambapo wanalazimika kulipia pesa ya dalali pale wanapopanga nyumba za kuishi au kwenye majengo ya kufanyia biashara ambayo imewaathiri kwa kiasi kikubwa.
Abboubakari Mhandeni ni mkazi wa Kigamboni katika jiji la Dar es salaam ambaye anafanya biashara zake katika stendi ya mabasi ya makumbusho ameeleza namna ambavyo alipata changamoto wakati alipohitaji eneo la kufanya biashara yake.
"Kiukweli hawa madalali wanatutesa sana kwa sababu ili upate chumba au sehemu ya kupanga unalazimika kumlipa pesa ya mwezi mmoja kutokana na bei ya nyumba mfano mimi wakati napanga hii frame nililipia kodi ya miezi sita pamoja na kumlipa dalali laki moja na nusu kwa hiyo unaweza kuona namna inavyotutesa". Alisema Abboubakari
Vile vile Lutigath Msengi ni mkaazi wa Kimara pia anaelezea namna ambavyo alipata misukosuko wakati anatafuta chumba cha kupanga ni pamoja na kuwalipa madalali mpaka ulifanikiwa kulipia kodi ya chumba alichokipenda.
"Yani mimi nilipata tabu sana kwa sababu sikupata chumba siku hiyo hiyo tulizunguka na madalali siku tatu hadi pale nilipopata chumba nilichokipenda na kila siku nilikua nawalipa elfu tano ya usumbufu na nilipopata chumba ndo nikatoa elfu arobaini ya mwezi mmoja". Alisema Lutigath
Abilahi Sudy aliongeza kua ili upate sehemu ya kupanga inatakiwa uwe na pesa ya miezi saba yaani sita ya mkataba wa chumba na ya mwezi mmoja ya dalali ambapo inakua ni changamoto kubwa hasa kwa vijana wadogo tunaoanza kujitegemea maisha.
"Ukisema utafute nyumba ya kupanga mwenyewe bila kumshirikisha dalali yani ni ngumu kupata kila unapoenda kuulizia unaambiwa vyumba hakuna kumbe vipo ilmradi tu umtafute dalali ili umlipe ela na kuna wenye nyumba wengine nao wanakua ni madalali pia kwa hiyo hawawezi kukupangisha chumba mpaka uwalipe na wao kwa hiyo inabidi uwe na hela miezi kupanga". Alisema Abilahi
Mmiliki wa nyumba Hassan Usanje ambaye ni mkazi wa Mwenge jijini Dar es salaam amesema kuwa suala la madalali ni muhimu kwao kwa kuwa linarahisisha upatikanaji wa wateja kwa haraka zaidi. Na kuongeza kua suala la malipoinategemea na maelewano ya dalali na mpangaji.
Michael Mpagama ni dalali ambaye anafanya shughuri zake katika maeneo ya Sinza pamoja na Kijitonyama amesema wao kama madalali wana chama chao cha madalali kinachopatikana sayansi Kijitonyama ambachokinawaongoza katika utendaji kazi wao. Vilevile ameongeza kuwa suala la malipo ni jukumu la mpangaji na si mmiliki wa nyumba kwa sababu mwenye uhitaji ni mpangaji hivyo Hana budi kulipia gharama za dalali.
"Suala la malipo ni jukumu la mpangaji kwa kuwa mpangaji ndiye mwenye shida hata wahenga walisema "mtaka cha uvunguni sharti ainame" hivyo analazimika kunilipa mimi kwa sababu natumia muda wangu kuzunguka nae ili apate nyumba". Alisema Michael
Katika ufafanuzi wake mjumbe wa serikali ya mtaa waMakenziuliyopo Buza jijini Dar es salaam Salma Omary Manevaamesema kuwa suala la madalali halitambuliki kisheria isipokuani makubaliano ya wenyewe kwa wenyewe bainabya dalali na mpangaji.
"Sisi kama serikali za mtaa hatuwatambui madalali, wanaendesha shughuri zao kulingana na makubaliano yaokati ya dalali na mtu anaetafuta nyumba. Ingekua kama tunawatambua ni lazima wangepitia ofisini kwetu katika kazi zao lakini wanamalizana wenyewe juu kwa juu". Alisema Bi Salma