Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Yakerwa na Mpangilio Mbovu wa Jiji la Mbeya

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Yakerwa na Mpangilio Mbovu wa Jiji la Mbeya

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imekerwa na mpangilio mbovu wa makazi katika Jiji la Mbeya huku kukiwa na kasi ndogo ya umilikishaji wa ardhi kwa wananchi waliopimiwa viwanja vyao.

Kamati hiyo ilionyesha kukerwa na mpangilio huo wakati ilipokuwa inahitimisha ziara yake Mkoani Mbeya baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa upimaji wa viwanja katika maeneo ya Iziwa na Ituha.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Ally Makoa ambaye ni Mbunge wa Kondoa Mjini, alisema katikati ya Jiji la Mbeya kuna nyumba zimejengwa lakini hazina hadhi ya kuwa kwenye Jiji na badala yake zilitakiwa kuwa vijijini.

Alisema Jiji kwa sasa linapima viwanja vya makazi mpaka kwenye milima wakati katikati ya Jiji kuna nyumba nyingi ambazo haziko kwenye mpangilio mzuri na hivyo akawataka kufanya utaratibu wa kuboresha makazi hayo.

Makoa alisema utaratibu wa upimaji wa viwanja katika Jiji hilo utasababisha matatizo ya migogoro ya ardhi na kuanza kuomba maeneo ya Hifadhi za misitu ili zipimwe kwa ajili ya makazi.

“Ujenzi wa kamazi haya tunayoyaona hapa katika Jiji la Mbeya ni wa kusababisha matatizo, kuna utafiti unaonyesha kuwa baada ya miaka kadhaa kila walipo watu 10, saba watakuwa wanakimbilia mjini, sasa hili jiji mnaendelea kujenga nyumba za chini ambazo zinachukua maeneo makubwa bila sababu,” alisema Makoa.

Hata hivyo alisema kwenye maeneo ya malango ya kuingilia katikati ya Jiji hilo watu wanapanda mazao marefu yakiwemo mahindi ambayo yanasababisha Sura ya Jiji kutokuwa nzuri.

Naye Mbunge wa Rorya, Jafary Chege alilitaka Jiji la Mbeya kuhakikisha linapopima viwanja liweke utaratibu wa kuweka mna miundombinu mingine ikiwemo barabara za mitaa ili kuwavutia wananchi kuchangamkia viwanja hivyo.

Alisema taarifa za uuzaji wa viwanja katika Jiji hilo zinaonyesha kuwa jiji hilo linabakiza sh. 1000 kwenye kila mita moja ya kiwanja kulingana na bei zilizopangwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya makazi na hivyo akautaka uongozi wa Jiji hilo kutumia fedha hizo kusogeza huduma.

Alisema huduma zingine muhimu zinazotakiwa kusogezwa kwenye viwanja vinavyopimwa ni maji, umeme na huduma zingine muhimu za kijamii ili wananchi watakaojenga kwenye viwanja hivyo wasianze kuhangaika tena kupata huduma hizo.

“Mnapopima viwanja lazima mvifanye viishi kwa kuhakikisha wananchi wanajenga na kuishi, njia pekee ya kuyafanya kuwa hai ni kusogeza huduma za kijamii hasa maji na umeme,” alisema Chege.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aloyce Kwezi aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo hasa zinazohusiana na shughuli zinazohusu shughuli za ardhi.

Alipongeza idara ya ardhi kwa kuhakikisha maeneo yanayopimwa yanaendelewa kwa kuzingatia sheria huku akikipongeza Chuo cha Ardhi kwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi.

“Maagizo ya Kamati kwenu ni kuhakikisha mnasimamia vizuri maeneo haya ili yajengwe kulingana na mahitaji ya kila eneo, isije ikatokea tena mkawa mnahangaika kupima maeneo lakini hati hazitolewi kwa wananchi,” alisema Kwezi.