Imani Potofu Bado Kikwazo Utunzaji Mazingira na Mipango Miji katika Jiji la Mbeya

Imani Potofu Bado Kikwazo Utunzaji Mazingira na Mipango Miji katika Jiji la Mbeya

IMANI potofu, miongoni mwa jamii za wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, zimetajwa kuwa ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji hovyo wa misitu hali inayoathiri maisha ya viumbe hai.

Chifu wa Kabila la Wasafwa, Roketi Mwashinga aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na Mwandishi wa habari ambapo alisema ni wajibu kwa viongozi wa kimila katika kupambana na uharibifu wa mazingira sambamba kuwakumbusha wananchi kuzingatia mipango miji.

Alisema imani potofu ambazo zinaaminisha watu kuwa baadhi ya uoto ni utajiri umechangia kwa kiasi kikubwa kupoteza uoto wa asili na kusababisha jangwa au ukame na kusababisha wananchi kuvamia makazi ya watu.

“Laiti machifu au wazee wa vimila wangekata miti hovyo au kuharibu maliasili kizazi cha sasa kisingenufaika na uoto wowote wa asili na huenda kungekuwa ni jangwa ndio maana tumeamua kulivalia njuga ili kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira,” alisema Mwashinga.

Aliongeza kuwa zipo baadhi ya imani kuwa kuchoma misitu kunasaidia kupata mazao mengi mashambani pamoja na kuwakamata kirahisi wanyama wa porini kwa ajili ya kitoweo na kwamba imani hizo zinaharibu ikolojia.

Alisema imani za aina hiyo ni za uongo na hazina faida yoyote kwa binadamu zaidi ya kuharibu mazingira ambayo ndiyo makazi ya viumbe hai mbalimbali wakiwemo wanyamapori, mimea mbalimbali, ndege pamoja na wadudu ambao wanapendezesha mazingira.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Stephen Katemba alisema elimu ya utunzaji wa mazingira na kuzingatia miongozi inayohamasisha masuala ya mipango miji ambayo inatolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imesaidia kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira wilayani humo.

Alisema kwa sasa wamefanikiwa kudhibiti vitendo vya uchomaji misitu hovyo na kwamba wananchi wameanza kuelewa madhara ya matukio hayo na wanamasishana wao wenyewe kulinda misitu .

Aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la upandaji miti jambo ambalo limesaidia utunzaji wa kimazingira na kwamba wanategemea elimu hiyo itasaidia kuifanya wilaya hiyo kuwa kinara utunzaji mazingira nchini.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya hiyo walisema kutokana na elimu waliyoipata ya utunzaji wa mazingira, watahakikisha wanalinda mazingira hasa misitu ili waondokane na matatizo ambayo yamekuwa yakiwakabili ikiwemo ukosefu wa maji.

Mmoja wa wananchi hao, Ambokile Samwel alisema tangu walipoanza kupewa elimu wamekuwa na mwamko wa kulinda mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kwa kupanda miti na kuzuia mifugo kuingia kwenye maeneo hayo pamoja na kuhakikisha kila mmoja anashiriki kuzuia moto.