Wafugaji Mbarali Washauriwa Kutenga Maeneo ya Mifugo ili Kuondokana na Migogoro
WAFUGAJI wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wameshauriwa kununua ardhi kwa ajili ya kuchungia mifugo yao badala ya kutegemea maeneo yaliyotengwa na Serikali ili kuondokana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiibuka mara kwa mara.
Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya hiyo, Reuben Mfune, ambapo aliwataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kwenye hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili kuepusha migogoro ambayo husababisha mapigano ya mara kwa mara.
Alisema maeneo yaliyotengwa na Serikali hayatoshi kwa ajili ya matumizi ya wafugaji na wakulima hivyo kufanya maeneo yaliyotengwa na Serikali na makazi ya watu kuvamiwa.
“Mfugaji ambaye umeamua kufuga mifugo mingi unatakiwa ununue ardhi yako na hiyo itasaidia kuhifadhi na kutunza mazingira kwa sababu kila mmoja atakuwa na uchungu, sitakubali kuona maeneo yaliyotengwa na serikali yanaharibiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo,” alisema Mfune.
Baadhi ya wafugaji walimweleza Mfune matatizo yanayowakabili ikiwemo uhaba wa maeneo ya kuchungia huku wakiomba Serikali kulifuta Tangazo lake namba 28 la mwaka 2008 (GN 28) ambalo lilipanua Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na hivyo kupunguza maeneo ya kuchungia.
Mmoja wa wafugaji hao, Shaban Olelengananu, ambaye ni mfugaji wa Kijiji cha Mwanavala alisema Kijiji hicho kina eneo la wafugaji ambalo lilipimwa wakati wa uwekaji wa matumizi bora ya ardhi lakini limevamiwa na wakulima.
Alisema hali hiyo imewafanya wafugaji kukosa maeneo ya kuchungia na kwamba wakitaka kuchungia katika eneo hilo inaibuka migogoro na wakulima ambao alidai ndio wavamizi.
“Sisi wafugaji tunakuwa kama hatuhitajiki katika Wilaya hii, watu wa Tanapa wanatuzuia kuchungia kwenye hifadhi, wakulima nao wamevamia eneo letu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na Serikali,” alisema Olelengananu.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, Hashim Mwaliaga, alimuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kufikisha kilio cha wananchi wa Wilaya hiyo ili mipaka ya hifadhi irekebishwe.
Alisema GN 28 ndio chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo kwa maelezo kuwa imechukua maeneo mengi ya wananchi wilayani humo na kuyafanya kuwa sehemu ya hifadhi.