Ijue Sheria ya Mipango Miji ya Mijini na Vijijini

Ijue Sheria ya Mipango Miji ya Mijini na Vijijini

UENDELEZAJI wa Miji nchini Tanzania,  unaongozwa na Sera ya Maendeleo ya Makazi ya Taifa pamoja na Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 ya mwaka 1956 iliyorekebishwa mwaka 1961.

Kwa mujibu wa Idara ya Mipango Miji na Vijijini  inaeleza kuwa shughuli zote za uendelezaji wa makazi zinatekelezwa na Halmashauri husika za Wilaya, Miji, Manispaa na Jiji na usimamizi upo chini ya Waziri mwenye dhamana ya  Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi nchini.

 Majukumu ya wizara kuhusu uendelezaji wa miji  ni kuandaa Sera na Sheria za  kuendeleza Miji na kusimamia utekelezaji wake,  kuandaa Mipango ya jumla ya kuendeleza miji (Master plans na Interim Land use plans), kuandaa mipango ya kuendeleza maeneo ya kati ya miji (Urban Rewal plans), kukagua na kuidhinisha michoro fasaha ya uendelezaji miji (detail layout plans), kushirikiana na Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji.

Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi inyoandaliwa na Mamlaka mbalimbali, kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya Sera, Sheria na Kanuni zinazokinzana. kuandaa miongozo, maagizo na kanuni za upangaji ardhi wa Vijiji,Miji Wilaya, Mikoa na Taifa.

Upangaji wa Ardhi ya vijiji ni chimbuko kuu la uchumi wa Tanzania kwa kuwa wakulima wengi wanaishi huko na kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii  ili kuwepo na mwongozo wa uendelezaji mzuri wa ardhi vijijini, wilayani na mkoani, kunahitajika mipango thabiti ya matumizi ya ardhi.

Mamlaka mbalimbali zikiwemo Serikali za Vijiji, timu za Wilaya za kupanga ardhi na Baraza la Taifa la kupanga matumizi ya ardhi huandaa mipango shirikishi katika ngazi ya Kijiji, Mkutano wa Kijiji una nguvu na unatosha kupitisha mpango wake wa kijiji husika  kwa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya, Mkoa na Taifa lazima mipango hiyo uwasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana ya uendelezaji wa ardhi ili na auidhinishe.

Hatua zinazotakiwa kufuatwa ni  Michoro au mipango ya matumizi ya ardhi huwasilishwa Wizarani na Mamlaka mbalimbali za upangaji wa ardhi, mipango hupokelewa Wizarani ambapo Kurugenzi ya Mipangomiji, Sehemu ya vijiji itapitia na kuchambua mipango hiyo na kutoa mapendekezo, Idara hupendekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya ardhi kupitisha au kukataa mipango husika.

Mipango hiyo hurejeshwa tena kwa wahusika kwa utekelezaji na Kumbukumbu za michoro hiyo huhifadhiwa kwa rejea za baadae.

 Usanifu Miji 

 Michoro ya maeneo ya Makazi huandaliwa na Halmashauri husika na huidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji Wizarani, Wizara hushiriki katika maandalizi pale tu ambapo Halmashauri itakapohitaji watalaam wa kuimarisha uwezo kiutendaji katika utekelezaji wa jukumu hilo, utaratibu ufuatao ndio hufuatwa na Halmashauri katika kuandaa michoro husika.

Kutambua eneo na kulitangaza kwenye gazeti la Serikali, kuwajulisha na kuhamasisha wananchi walio ndani ya eneo lililotambuliwa, kufanya uthamini wa maendelezo ndani ya eneo na kulipa fidia, kubuni michoro ya makazi na matumizi ya ardhi na kuiwasilisha kwenye Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ili ijadiliwe na kupitishwa.

 Michoro huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya Maendeleo ya Makazi ili iidhinishwe na Mkurugenzi wa Mipango Miji.

Kuandaa Mipango Kabambe 

Maandalizi ya Mipango hii hufanywa na Halmashauri husika za Miji, Wilaya, Manispaa na Jiji kwa kushirikiana na Wizara  kutoa wataalamu wa Kujenga uwezo wa Halmashauri hizo kufanya kazi hiyo.

Maandalizi ya Mipango hii hufuata utaratibu ukiwemo uhamasishaji wa Madiwani, Watendaji na watoa huduma muhimu za kijamii, kiuchumi na kitaasisi, uandaaji wa Ramani ya Msingi (base map), ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi na tathmini ya takwimu za kimaendeleo na kimazingira, maandalizi ya rasimu ya mpango na ramani husika,  kufanya Mkutano Mkuu wa majadiliano/mashauriano na wadau husika.

 Uainishaji wa masuala muhimu ya kijamii, kiuchumi na kimazingira, kuandaa mpango endelevu wa mji pamoja na michoro/ramani husika,  kuwasilisha mpango kwa wadau wa Halmashauri kwa maafikiano ya kukubaliwa au kukataliwa, mpango huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya Mipango miji na kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji.

Kusimamia/ Kudhibiti Uendelezaji Miji 

Katika eneo hili Wizara hutekeleza yafuatayo, kutafiti na kutangaza viwango vya mahitaji ya ardhi kwa matumizi mbalimbali, kutangaza maeneo yaliyoiva kuendelezwa kimji baada ya kujadiliana na Halmashauri husika, kuidhinisha/ kukataa maombi ya kubadili matumizi ya ardhi yaliyowasilishwa kutoka kwenye Halmashauri.

Mwananchi azingatie kuwa maombi yanafanyika katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri lilipo eneo husika. Wizara ya Ardhi itahusika katika kuidhinisha michoro ya mipango miji, ramani za upimaji na kwenye hatua ya hati.